Configure HTML/JavaScript Fire & Rescue Singida Official Blog: HISTORIA YA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI TANZANIA

Saturday, May 9, 2015

HISTORIA YA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI TANZANIA



Kutoka “Police Fire Brigade” Hadi
    “Jeshi la Zimamoto Tanzania”
·                    Sheria namba 14 ya mwaka 2007, chachu ya ufanisi wake
·                    Lanufaika na ushirikiano na JWTZ
Na Sgt.Hassan J.Mtengevu
Huduma za Zimamoto Tanzania Bara zilianza wakati wa utawala wa kikoloni mara baada ya vita kuu ya pili ya dunia mwaka 1945, ambapo kipindi hicho kulikuwa na kikosi kimoja tu kilichoitwa Police Fire Brigade kilichosimamiwa na Jeshi la Polisi.
Mwaka 1950 huduma hii iligawanywa katika makundi mawili ambayo ni Zimamoto ya Manispaa iliyokuwa chini ya usimamizi wa Manispaa, na Zimamoto Viwanja vya Ndege iliyokuwa chini ya usimamizi wa Idara ya Kazi.
Kutokana na kupanuka kwa miji, viwanja vya ndege na bandari, vikosi vingine vya Zimamoto vilianzishwa na kimojawapo ni Zimamoto Bandari chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari.
Mwaka 1982 huduma ya Zimamoto viwanja vya ndege iliwekwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakati vikosi vya Zimamoto vya Manispaa na Miji viliwekwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, vikisimamiwa na Wizara ya Serikali za Tawala za mikoa na Miji.
Kutokana na majukumu ya Zimamoto kusimamiwa na mamlaka tofauti, ufanisi wake haukuwa wa kuridhisha, hivyo kuilazimu serikali kuangalia namna ya kuboresha huduma hiyo.
Mwaka 1985, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria Na. 3 iliyoanzisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuifanya huduma hiyo itolewe katika nidhamu ya kijeshi chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Katika kuendelea kuboresha huduma za Zimamoto na Uokoaji, mwaka 2007 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria Na. 14 ya Zimamoto na Uokoaji yani (Fire and Rescue Force Act) iliyoviweka vikosi vya Zimamoto na Uokoaji chini ya kamandi moja.
Sheria hii kwa kiasi kikubwa ilitoa fursa kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji kujipanga upya kimuundo na kuweka mgawanyo wa majukumu wenye tija, ili kurahisisha utoaji huduma ya zimamoto na uokoaji.
Sasa hivi jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaongozwa na Kamishna Jenerali anayesaidiwa na Naibu Kamishna Jenerali, akifuatiwa na Makamishna watatu wanaoongoza divisheni tatu za jeshi hilo ambazo ni utawala na fedha, oparasheni na tawi la usalama wa umma na mali.
Chini ya divisheni hizi kuna vitengo vinavyoongozwa na Makamishna Wasaidizi, ili kutengeneza mfumo wa kiutendaji wenye kuleta tija katika utoaji huduma kwa jamii.
Divisheni ya Usalama wa Umma linahusika na kuzuia na kukabiliana na majanga kama moto, matetemeko ya ardhi, mafuriko, na majanga mengine pindi yanapo tokea pamoja na kufanya uchunguzi wa majanga hayo kubaini chanzo chake na kupanga mikakati ya kukabiliananayo.
Kupitia vitengo vilivyo chini yake, pia divisheni hii linahusika na kuelimisha jamii juu ya majanga ya moto na uokaoji, kukagua majengo, kuandaa na kutekeleza mipango ya kuzuia moto, kupanga na kukagua usalama wa ujenzi katika viwanda, vituo vya mafuta na kemikali pamoja na vituo vinavyozalisha gesi.
Kwa upande wa divisheni ya oparesheni, miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia mafunzo, kukagua huduma za zimamoto na uokoaji kwenye kanda pamoja na kufanya tahmini ya madhara yaliyotokea kwenye majanga mbalimbali.
Majukumu ya divisheni ya Utawala, rasilimali watu na fedha ni kufanya utafiti na mafunzo, kusimamia uajiri, kuandaa na kutunza kumbukumbu za watumishi pamoja na maandalizi na mapitio ya sheria ya moto na uokoaji na kanuni zake.
Pamoja na muundo huo, Jeshi la Zimamoto pia limeweza kuboresha chuo chake ambacho majukumu yake ni kuendeleza na kufanya mapitio ya muundo wa Zimamoto na Uokoaji, kufanya utafiti kuhusu madhara ya matukio ya majanga ikiwa ni pamoja na kulinganisha matokeo ya ndani na nje ya tafiti hizo.
Chuo hiki pia kinatoa mafunzo yote kwa askari wa Jeshi hilo pamoja na mafunzo ya nidhamu kwa maafisa, sambamba na mafunzo kwa wadau majanga mbalimbali wote pamoja na wananchi kwa ujumla.
Pamoja na changamoto kadhaa zinazolikabili Jeshi la Zimamoto, Jeshi hilo kwa kiasi kikubwa limejitahidi kusambaza huduma zake kwa wananchi, kwa kweka vituo vya zimamoto katika baadhi ya makao makuu ya mikoa, wilaya na maeneo mengine muhimu nchi nzima.
Mafanikio mengine ni Jeshi hilo kuwa na ushirikiano mkubwa na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, hivyo kuongeza wigo wa kiutendaji. Miongoni mwa matunda ya ushirikiano huo ni pamoja na Jeshi la Magereza kukubali kutoa mafunzo ya kijeshi ya awali, uongozi mdogo wa kati na uongozi wa juu ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji maafisa na askari wa Zimamoto.
Kwa upande wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, limekuwa karibu sana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika maokozi pindi yanapotokea majanga makubwa yanayotishia usalama wa watu na mali zao.
Kwa mfano tarehe 03 Desemba 1989 Jeshi la Wananchi lilishirikiana na Zimamoto na Uokoaji kukabiliana na moto uliotokea katika kampuni ya kusafisha mafuta ya Tazama Tank Farm Dar es Salaam na kufanikiwa kuuzima. 
Mwaka 2001 vyombo hivyo vilishirikiana tena kupambana na moto wa mafuta uliotokea katika kinu cha kufua umeme yaani cha TANESCO eneo la  Ubungo Dar es salaam na kufanikiwa kuuzima na kuokoa maisha na mali za wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Maeneo mengine ni pamoja na ajali za MV SPICE ISLAND NA MV SCAGIT zilizotokea Zanzibar.
Ushirikiano huu umeenda mbali zaidi ambapo ili kuzidi kusambaza huduma za zimamoto kwa wananchi, JWTZ limeridhia kuruhusu ujenzi wa vituo vya Jeshi la Zimamoto kwenye baadhi ya maeneo ya kambi zake za Lugalo, Mabibo, Kigamboni, Mbagala na Gongolamboto.
Hii inatokana na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange kwa kushirikiana na watendaji wa Jeshi hilo, kuwathamini watanzania na mchango wa Jeshi la Zimamoto kwa jamii.
Kwa hakika pamoja na kwamba historia ya Zimamoto inaonesha Jeshi hilo lilianza kwa kusuausua, kwa jitihada za Serikali katika kurekebisha sheria na mazingira ya utendaji wa Jeshi hilo na kwa ubunifu wa watendaji wa Jeshi hilo katika kuliboresha, leo hii watanzania wameanza kunufaika na huduma yake.
Kilichopo sasa ni kwa kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha changamoto zinazolikabili jeshi hilo zinapatiwa ufumbuzi, ili kuliboresha Jeshi hili kwa rasilimaliwatu na vifaa hatimaye Taifa liwe na uwezo wa kukabiliana na majanga yanayohatarisha usalama wa watu na mali zao.
Imeletwa kwenu kwa hisani na usaidizi wa Cpl Ibrahim Luena.
©Public Relation Education and Information-Fire and Rescue Singida


1 comment:

  1. Hakika tunafurahia huduma za jeshi la zimamoto, japo kuna changa moto ndogondogo za kiutendaji hasa kwa askari wa jeshi hilo;
    1. askari kujihusha kutoa huduma zinazotolewa na na madelear ambao wapo kisheria na wanalipia vibali halali vinavyotolewa na jeshi ( certificate of competence)
    na wanasahau majukumu yao ya msingi kabisa.

    ReplyDelete